KRISMASI ni sherehe ya KIKRISTO kwa sababu ni tukio la kukumbuka
kuzaliwa kwa Kristo, Yesu, mwokozi wa Ulimwengu! Kwa hiyo hata kama si
agizo katika Biblia, lakini kitendo chochote kinachomhusu Yesu Kristo,
kikifanyika na waKikristo, tayari kinatosha kuwa ni tukio la Kikristo.
Kwa hali ya kawaida Siku hii haiwezi kuadhimishwa na waislam,
wabudha, wahindu, na wengine ambao msimamo wa imani zao haupo
katika UKOMBOZI ulioletwa na Mungu kupitia Yesu Kristo.
Kwa wote wanaokubali kwamba Kalenda ya sasa tunayoitumia ni ya
uhakika na huwa haikosei, basi lazima akubali kwamba Yesu Kristo
alizaliwa Desemba 25. Wala huna haja ya kubisha.
Soma Maandiko vizuri. Maandiko yanaonesha kwamba wayahudi walikuwa na
desturi ya kuwatahiri watoto siku ya nane baada ya kuzaliwa. Ukisoma
maandiko yanaoenesha kwamba Yohana Mbatizaji alitahiriwa siku ya nane
baada ya kuzaliwa. Watoto wote wa kiyahudi walitahiriwa SIKU YA NANE.
YESU NAYE ALIPELEKWA KWENYE TOHARA SIKU YA NANE BAADA YA KUZALIWA. (Luka
1:59, 2:21)
Nanukuu, ” Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri aliitwa jina lake Yesu……..” Luka 2:21
Wote wapendwa mtakubali kwamba siku ya nane ambayo imetajwa huwa ni
tarehe moja mwezi wa kwanza. Hii kusherehekea sikuu kuu ya mwaka mpya
kwa ufupi ni sherehe iliyopaswa kusherehekea KUTAHIRIWA KWA YESU.
Kwani
alizaliwa tarehe 25 Desemba na ukihesabu kuanzia tarehe 25 Desemba hadi
tarehe moja mwezi wa Kwanza ni siku nane.
Katika sikukuu
zinazosherehekewa kwa msisimko mkubwa duniani, hakuna inayofikia
Krismas. Utafiti unadhihirisha kuwa sikukuu hii inasherehekewa kwenye
mataifa mengi duniani kama sikukuu ya kidini na pia ya kitaifa (public
holiday). Hii hufanywa hata na baadhi ya mataifa yasiyofuata mwelekeo
wowote wa dini. Mambo yafanyikayo katika sikukuu hii mfano, kupambwa kwa
mti wa Krismas, kubadilishana zawadi, kutembeleana n.k, yana mizizi
yake tokea mbali sana kihistoria. Dunia imekuwa ikisherehekea siku hii
kama kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo.
Lakini ni wachache sana duniani wanaofahamu kuwa kwa kweli Yesu hakuzaliwa tarehe 25 Desemba, wala kwamba
tarehe hiyo haina uhusiano wowote na ujio wake duniani. Labda la
kushtua zaidi ni ule ukweli kuwa siku hii ilianza kusherehekewa kwa mara
ya kwanza mwaka 350 BK (wengine husema ni 354 BK) kama siku ya kuzaliwa
kwa Yesu ikiwa na lengo la kubadilisha sikukuu ya kipagani ya
Saturnalia iliyokuwa ikiheshimiwa sana siku za dola ya Rumi, kuwa
ya Kikristo.
Pengine utaniuliza, “kama ni hivyo, je, mchungaji huoni
kuwa ni makosa kabisa kusherehekea Krismas kwa kuwa ni kama kuabudu
miungu ya uongo, tena ni kudanganya kuwa ni ‘birth day’ ya Yesu wakati
sivyo?” Hili ndilo swali na hoja ya wengi wasioamini kuwa ni sahihi
kuadhimisha Krismas, na ndiyo maana natamani tujadili leo, ili tuone
maana ya kweli ya Krismas na umuhimu wake kwa waamini wa kweli leo. Neno
kuu tutakalojifunza hapa ni ule ukweli kuwa Krismas sio siku, ila ni
ujumbe tuupatao kutokana na lile tukio la kuja kwa Mwokozi duniani.
Kama mtu akiitazama Krismas kama siku na akaadhimisha siku hiyo kama “birth day” ya Yesu, kama
ni mtafiti wa mambo atagundua haraka sana kuwa amekuwa akiadhimisha
siku ambayo siyo yenyewe. Lakini baya zaidi, atakuwa amekosa ile maana
yenyewe ya tukio la ujio wa Yesu duniani, na hivyo kuadhimisha kwake
kutakosa maana. Kwa sababu hii vyema tujifunze undani wa Krismas ili
tunaposherehekea tusiwe kama wachezao ngoma wasioijua. Kwa kuanza hebu tuangalie kwa ufupi maana ya neno “Krismas” na historia yake.
Neno
“Krismas” wala tarehe ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu havipo kwenye Biblia.
Hatuna budi kurejea historia ya Ukristo tuone asili ya neno na historia
yake. Huku kutokuwapo mambo haya kwenye Biblia kwenyewe kunaonesha dhahiri
kuwa Roho wa Bwana hakuona umuhimu wa kutilia uzito kwenye siku au
tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu, ila alitilia uzito kwenye tukio na ujumbe
wa tukio lenyewe, kama walivyoandika Mathayo na Luka.
Kama tutakavyoona, hata kanisa la kwanza halikutilia mkazo kwenye
tarehe au siku ya kuzaliwa kwake, ila maana na uzito wa ujio wake. Hebu
tuone ituambiavyo historia kuhusu Krismas:
Maana ya Neno Krismas na Historia yake
Neno
"Krismas" kama linatokana na neno la kiingereza "Christmas" ambalo
likitafsiriwa moja kwa moja (transliteration) linakuwa "Christ's Mass"
ikimaanisha "Kusanyiko la Kristo." Kwa mujibu wa encyclopedia ya
Wikipedia, tarehe au mwaka wa kuzaliwa kwa Yesu hasa haujulikani,
ila inakisiwa ni kati ya mwaka 7-2 BK. Kabla ya mwaka 350 BK siku ya
kuzaliwa kwa Yesu iliadhimishwa tarehe 6 January. Mwaka huo (350) kwa
uamuzi wa kanisa la Rumi tarehe 25 Desemba ilianza kutumiwa kama sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu. Hii ni kwa mujibu wa kitabu cha Earle E. Cairns kiitwacho Christianity Through the Centuries (1954, 120).
Kabla
ya hapo tarehe hiyo ilitumiwa na wapagani wa Rumi kuabudu mungu wao
aliyeitwa Saturn. Katika ibada ya Saturnalia watu walipamba miti, na
kupelekeana zawadi. Wengine walitembea uchi mitaani, vitendo vya
uasherati na kuua, vilikuwa sehemu ya ibada hiyo. Wapagani hao
walipotakiwa kuacha upagani na kuukubali ukristo waliona kuwa kikwazo ni
kuacha kuadhimisha siku ya Saturnalia. Kanisa la Rumi likawaruhusu
waabudu siku hiyo lakini sio kama kwa mungu Saturn, bali kama
kuadhimisha kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo. Hii inashuhudiwa na
wanahistoria wengi sio Cairns pekee. Leo ukifanya utafiti kidogo tu
kwenye google utakutana na hilo kwa wingi sana.
Kilichofanywa
na kanisa la Rumi, yaani kuwaingiza wapagani kanisani kwa kutengenezea
sikukuu inayoendana na siku yao ya kipagani kuliifanya hatimaye ibada
yao ya kipagani ife kabisa. Lakini kwa kweli hakukuwabadilisha mioyo yao
wala hawakugeuka kuwa Wakristo wa kweli. Walipokea dini kama dini
lakini sio uzao mpya mioyoni mwao. Historia inatuambia kuwa wapagani hao
walikuwa wanasherehekea sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kanisani, lakini
wakitoka kanisani vile vitendo vya kipagani waliendelea navyo kama
kawaida. Hii ni kusema kuwa siku pekee haitoshi kumbadilisha mtu, wala
kuadhimisha siku hakumuokoi mtu yeyote.
Tuseme
nini basi kwa habari ya siku ya terehe 25 Desemba kuwa Krismas, yaani
kusanyiko la Kristo linaloadhimisha kuzaliwa kwa Mwokozi Yesu? Je,
kwa kuwa mwanzo wake kihistoria ni dhaifu kiasi hicho ni dhambi
kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu. Je, tunapoadhimisha Krismas tarehe hii ya
leo huku tukijua kuwa kweli Yesu hakuzaliwa tarehe kama hii ya leo
tunamkosea Mungu wetu? Je, tufanyapo haya tunajiunga na wale wapagani
kuabudu mungu Saturn kama wengine wasemavyo? Je, tuache kabisa kutambua
kuzaliwa kwa Yesu.
Jibu
la hayo yote lipo kwenye kutofautisha kati ya kuiadhimisha siku kama
siku, na kuadhimisha tukio la kuzaliwa kwa Mwokozi Yesu. Kama tukitukuza
siku ya tarehe 25 Desemba, kana kwamba ni siku takatifu ya kuzaliwa kwa
Yesu, na kuadhimisha kwetu tukakujenga kwenye siku kama vile ni
"birthday ya Yesu" tutakuwa tunakosea. Kwanza kwa sababu uzito wa kuja
kwa Yesu haupo kwenye siku au tarehe ya kuja kwake bali kwenye maana na
ule ujumbe utokanao na kuja kwake. Pili kwa sababu siku au tarehe
haituongezei wala kutupunguzia kitu chochote kiroho hata tuitukuze na
kuiadhimisha. Kama ingekuwa muhimu kiasi hicho basi Biblia ingetuwekea
mazingira ya kujua tarehe ya kuzaliwa kwake na kutuagiza tuiadhimishe,
lakini iko kimya kwa habari hiyo. Tatu sio sahihi kusema kuwa Yesu
alizaliwa tarehe ambayo hakuzaliwa.
Lakini
kama tukiiona tarehe 25 Desemba kama siku tuliyoitenga kutafakari tukio
la kuja kwa Yesu Kristo duniani, siyo kwa sababu ndiyo tarehe
aliyozaliwa, wala siyo kwa lengo la kuwafanya wapagani waukubali Ukristo
kama lilivyofanya kanisa la Rumi, bali kwa sababu kuzaliwa kwa Yesu
kuna umuhimu na uzito unaostahili na unaokubalika kibiblia kusherehekewa
na kuzingatiwa na wafuasi wa kweli wa Kristo tunatenda vyema, naam,
vyema sana.
Neno
kubwa hapa ni ule mtazamo tunaokuwa nao kuhusu ile siku, kunakotokana
na mahali , yaani hatua tulipo kiroho. Mara nyingi watu walio wachanga
kiroho wanapofahamu kuwa kumbe tarehe
ya kuzaliwa kwa Yesu siyo hii, na ya kwamba mazingira yaliyopelekea
hata tarehe hiyo itumike kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu ndiyo hayo,
dhamiri zao changa hutishiwa usalama, wakidhani kuwa wakiadhimishisha
Krismas watakuwa wanaabudu miungu au watakuwa wanasema uongo. Lakini
tukumbuke kuwa hakuna siku ya shetani, bali siku zote ni za Bwana.
Kwamba kuna watu waliowahi kuabudu miungu siku au tarehe fulani
kihistoria, hakutuzuii leo kumwabudu Mungu wetu siku au tarehe hiyo.
Tusifanye makosa ya kumkabidhi shetani siku.
Kama
kanisa la Rumi lingewapa Injili ya kweli wale wapagani, wakaokoka,
kisha wakawaambia kuwa badala ya kufuata ibada mfu za Saturnalia,
afadhali siku hiyo mtafakari wema wa Mungu wetu aliyetupenda hata
akatuletea zawadi ya Mwanawe wa pekee atuokoe, wangefanya vyema. tatizo
halikuwa kwenye kubadilisha siku kutoka kuwa siku ya kumwabudu shetani
kuwa siku ya kumwabudu Bwana. Tatizo lilikuwa kuwapa wapagani siku
kidini badala ya Yesu mwenyewe aokoaye.
Ujumbe wa Krismas ni Neema ya Mungu sio Siku
Ni
sahihi kusherehekea Krismas, tena inapasa, kwa nini? Kwa sababu kwanza,
mbingu zinatupa mwongozo huo. Alipozaliwa Yesu Mungu alifanya "Krismas"
ya kwanza kwa kupeleka Malaika kondeni walikokuwa wakichunga kondoo
wachungaji. Unakumbuka ujumbe wa Malaika hao? Hebu tukumbushane
walivyosema:
Malaika
akawaambia, "Msiogope, kwa kuwa mimi nawaletea HABARI NJEMA YA FURAHA
KUU ITAKAYOKUWA KWA WATU WOTE, maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa
KWA AJILI YENU Mwokozi ndiye Kristo Bwana"....Mara walikuwapo pamoja
huyo Malaika, wingi wa jeshi la Mbinguni wakimsifu Mungu na kusema;
Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia
(Luka 2:10-14).
Hii
ndiyo krismas ya kwanza, na kama unavyoona ilifanywa na Malaika. Mkazo
wao ulikuwa nini? Je ni siku? la sivyo. mkazo wao ulikuwa: "habari njema
ya furaha kuu wa watu wote." Hii habari njema ni kwamba amezaliwa kwa
ajili ya kila mtu Mwokozi, Kristo Bwana, hii ina maana kuwa dunia
imempata mmoja mwenye uweza wa kumwokoa kila mtu na dhambi zake, taabu
zake, na kumpa kila aliyekata tamaa tumaini jipya la uzima wa milele.
Hii ina maana kuwa kila mwenye dhambi sasa aweza kupokea uzima bure na
kuifanya mbingu kuwa nyumbani kwake. Siku ile aliyozaliwa Bwana ilikuwa
ni mapambazuko mapya, ilikuwa ni asubuhi mpya kwa dunia iliyokuwa
imewekwa kwenye giza la uvuli wa mauti tangu alipoanguka Adamu baba yetu
dhambini. Jua la haki lilizuka likiwa na uponyaji katika mbawa zake,
Jua hilo ndiye Yesu, aliyefanyika kuwa jibu kwa kila nafsi iliyochoka,
na isiyo na matumaini. Krismas inatuonesha neema kuu ya Mungu
aliyetujilia tukiwa wafu kiroho, na waliohukumiwa kwenda jehanamu ya
moto, na kutuletea wokovu huu mkuu kwa mkono wa Mwanawe Yesu Kristo.
Huu
ndio ujumbe wa Krismas, na ndio tupaswao kuusisitiza, sio siku. Aha,
hivyo basi kumbe kwa Mkristo wa kweli, Krismas ni kila siku, ila tu siku
tuliyokubaliana kuitenga inatupa nafasi ya kuweka mkazo wa pamoja, na
mazingira ya kuuambia ulimwengu uache kutukuza siku na badala yake uinue
macho na kumtazama Yesu Kristo awaokoe, na kuwapa ushindi maishani
kwani yeye ndiye amani yetu. Waliompokea Yesu wanapokusanyika pamoja
mioyo yao huimba "atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa
watu aliowaridhia." Hao kama "kusanyiko la Kristo" ndiyo Krismas
yenyewe, siyo siku. Ikumbukwe kuwa Krismas ni "Christ's Mass" yaani
"kusanyiko la Kristo."
Hii
ina maana kuwa kwa mkristo wa kweli Krismas ina mikazo miwili; wa
kwanza ni mkazo wa kuelekea juu (vertical emphasis) na mkazo wa kuelekea
kwa watu (horizontal emphasis). Mkazo wa juu ni wa ibada. Huu unadai
kudumisha moyo wa ibada kwa Mungu na shukrani kwa neema yake
aliyotupatia kwa kumleta Kristo kwetu. Malaika walitazama juu wakisema
"atukuzwe Mungu juu mbinguni." Mkazo kwa watu unadai tuwapelekee wengine
hizi "habari njema kwa watu wote" ili nao wapate wokovu wapokee "amani"
ya mioyo yao na kufanyika sehemu ya "kusanyiko la Kristo" ambalo ndilo
Krismas ya kweli.
Wengi
siku hii ya leo, wanasherehekea Krismas kwa ulevi, uasherati, ugomvi,
na wivi. Katika hao, wengi wametoka makanisani mwao, wamepokea mahubiri
kwa makasisi, wachungaji, na mpadre ambao nao yumkini mkazo wa mahubiri
yao ni siku ya kuzaliwa kwa Mwokozi kuwa ni leo badala ya ile maana ya
kuja kwake. Ni wangapi walioenda kanisani leo wamezaliwa mara ya pili na
kuokoka? Wengine hata hawaamini kuwa kuna kuokoka duniani, lakini
wanadhani bado wanasherehekea Krismas. Hivi haya makusanyiko mengi ya
wasemao hakuna kuokoka, kisha wanadai kusherehekea Krismas hawajiulizi
kuwa wao ni Kusanyiko la nani? Au wamesahau kuwa Krismas ni "Kusanyiko
la Kristo?"
No comments:
Post a Comment