MWANAMKE MAKINI BLOG

Advertise Here

Tuesday, 25 November 2014

BUNGE LANG'ANG'ANIA MJADALA WA ESCROW


SPIKA  wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda amesema mjadala ndani ya Bunge kuhusu sakata la akaunti ya Escrow upo pale pale na hakuna mhimili mwingine wowote unaoweza kulizuia Bunge kufanya hivyo.


Spika ametoa muongozo huo baada ya kuombwa na Mbunge wa Bariadi Mashariki John Cheyo (UDP) mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.


Katika muongozo wake kwa mujibu wa kanuni ya 68(7) Cheyo amesema kuna taarifa kuwa sula hilo la Escrow ambalo Bunge linatakakujadili leo limepelekwa Mahakamani ili kuzuia Bunge kuendelea kujadili suala hilo.


Akitoa muongozo wake Spika amewataka wabunge kuacha kuishi kwa wasiwasi kwa kuwaeleza kuwa hakuna mtu anayeweza kulikataza bunge kufanya kazi yake. Spika Makinda  amesema hapo awali waliambiwa kuwa kuna kesi nyingi mahakamani ambazo zinahusiana na suala hilo la akaunti ya Escrow.


Amesema hata hivyo baada ya kufuatilia kesi hizo zote hakuna kesi mahususi inayohusu jambo ambalo Bunge linaenda kujadiliana juu ya sakata hilo la Escrow.


Spika Makinda amesema Bunge lina sheria zake za kinga na kama kutakuwa na muhimili mwingine ambao unakuwa na uwezo wa kuzuia bunge kufanya kazi yake basi hakutakuwa na Bunge.’


Hata hivyo Spika amesema mpaka leo asubuhi alikuwa bado hajapata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa PAC Zitto Kabwe kama wamekamlisha kazi yao kwani kikanuni ni lazima wakikamilisha kazi hiyo hutakiwa kumtaarifu Spika kwa barua ili naye aingize katika shughuli za Bunge. 


Aidha Makinda amesema pamoja na kuendelea na mjadala huo pia wabunge leo watapewa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa majina.


Spika amesema nia ya kugawa taarifa hiyo ya CAG kwa majina ni kuepukana na taarifa hizo kuwafikia watu wengine ambao si wabunge.

No comments:

Post a Comment