MWANAMKE MAKINI BLOG

Advertise Here

Tuesday, 4 November 2014

NHC MWIKO KULEWA SIFA ZA MAFANIKIO


MKUU wa mkoa wa Tanga, Luteni (Mstaafu) Chiku Gallawa, amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), lisilewa sifa wanazopewa kwa kufanya vizuri katika ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, badala yake waongeze bidii na kuyataka mashirika mengine nchini yaige mpango kazi wake kujiletea maendeleo yake.

Akizungumza wakati akifunga baraza Kuu la wafanyakazi wa shirika hilo mwishoni mwa wiki, mkuu huyo wa mkoa alisema kwamba kasi ya kujiletea maendeleo ya shirika hilo kwa dira yake ya miaka mitano ni kubwa na kwamba watu mbalimbali wamekuwa wakilisifia kwa kazi nzuri akiwemo Rais Jakaya Kikwete.

Amesema kwamba kama mashirika mengine yaliyopo hapa nchini yangefanya kazi kwa kasi kama lilivyo shirika la NHC, Tanzania ingekuwa mbali katika mabadiliko ya kiuchumi hivyo akalipongeza shirika hilo liendelee kufanya kazi zake kwa vile Watanzania wamekuwa na mahitaji makubwa ya makazi.

Awali Mwenyekiti wa mkutano huo, Francis Chilambo akisoma maazimio ya mkutano huo wa siku mbili, alisema kwamba ili kuondokana na dhana ya kulewa sifa, wameadhimia kwamba kutokana na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kuwavutia wengi kiasi kwamba shirika hilo limekuwa kioo cha Watanzania, miradi yao yote itajengwa kwa ubora unaotakiwa.

Mwenyekiti huyo katika maadhimio hayo wamempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi, Alphayo Kidata kutokana na kuwa mstari wa mbele na kushirikiana na shirika hilo katika kuandaa mpango mkakati wa shirika hilo wa 2015 ikiwemo kupatikana kwa hati katika eneo la Tanganyika Packers lililopo Kawe Jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment