WABUNGE wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wameridhia azimio la kumpongeza spika wa bunge hilo mheshimiwa ANNE MAKINDA kwa
kuchaguliwa kuwa rais wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF).
Akisoma azimio hilo bungeni mjini
Dodoma mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa
mheshimiwa MUSSA ZUNGU amemzungumzia mheshimiwa MAKINDA kuwa ni mzoefu wa
kutosha katika medani za siasa na uongozi kwa zaidi ya miaka 37 kwa kushika
nyadhifa mbalimbali kitaifa na kimataifa.
Amesema kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa
na rais JAKAYA KIKWETE za kuitangaza nchi ya Tanzania zilisaidia sana katika
mchakato wa kumnadi mheshimiwa MAKINDA kwa wajumbe wa mkutano na kufanikiwa
kushinda kwa kishindo bila ya kupingwa.
Wakiunga mkono azimio hilo baadhi ya wabunge
waliochangia wamempongeza mheshimiwa MAKINDA na kusema ni mtu anayestahili
kupata nafasi hiyo kutokana na uchapakazi wake.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini mheshimiwa ZITTO KABWE
amesema kwa mara nyingine tena Tanzania imeshamiri katika medani ya dunia kitu
ambacho kinaleta heshima kubwa na ni ishara ya mafanikio makubwa ya
kidiplomasia katika nyanja ya kimataifa.
Amesema kupata kwake nafasi hiyo kunaonyesha wazi
kuwa ni jinsi gani bunge la Jamhuri lilivyokuwa halikufanya makosa kumchagua
kuwa spika na kusema ana aamini atapeperusha bendera ya Tanzania vizuri
anakokwenda na kuwataka wabunge kumuunga mkono kwa kuwa ni mtu mzuri.
Kwa upande wake mbunge wa viti maalum mheshimiwa BERNADETA
MUSHASHU ameungana na wengine kumpongeza na kusema hawakukosea kumchagua kwa
kuwa sifa anazo kutokana na kuandaliwa na Taifa hili na kumuomba mungu ampe
uwezo mkubwa wa kupeperusha bendera ya Tanzania.
Mbunge wa viti maalum mheshimiwa RUKIA AHMED amesema
anaona fahari kutokana na ushindi huo na kwamba uteuzi huu haujaja bure bali
umekuja kutokana na juhudi kubwa alizonazo katika utendaji kazi wake wa
kutobagua dini,kabila wala vyama vya siasa.
Wakati huo huo mheshimiwa
MAKINDA amewataka wabunge wa vyama vyote vya siasa kuamka na
kubadilisha fikra zao ili wafikirie Maendeleo.
Mheshimiwa MAKINDA akitoa shukrani kwa wabunge
amesema Maendeleo sio Taifa bali yanapaswa kuanzia kwa wabunge
wenyewe kwa kuwa hivi sasa nchi nyingi duniani wanachosimamia ni
suala la uchumi na upo uwezekano wa Tanzania kama wasiposimamia msingi huo
ikabaki nyuma.
Amewataka kuamka na kusimamia suala hilo ingawa
mwaka huu ni mgumu kwa sababu wanaelekea kwenye uchaguzi lakini isiwe sababu ya
kuacha kufanya kazi na kuanza kupigana vijembe.
No comments:
Post a Comment