Siku ya Ukimwi Duniani inaadhimishwa kila tarehe 1 Desemba kama siku maalumu ya kupanua ufahamu kuhusu maafa yanayoletwa na ugonjwa wa Ukimwi.
Desemba mosi ilichaguliwa kuwa siku ya Ukimwi kutokana na tarehe hiyo kuwa ndiyo siku ambayo virusi cha Ukimwi kilitambulika rasmi mwaka 1981. Toka mwaka 1981 hadi 2007 watu zaidi ya milioni 25 wameshafariki kutokana na Ukimwi. Mwaka 2007 peke yake walifariki milioni 2, kati yao watoto 270,000.
Siku hiyo ilichaguliwa rasmi mwaka 1988 wakati wa Mkutano wa Dunia wa Mawaziri wa Afya Kuhusu Mpango wa Kuzuia Ukimwi. Kuanzia hapo siku hiyo imekuwa ikikumbukwa rasmi na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wanaharakati.
Toka mwaka 1988 hadi 2004, Siku ya Ukimwi Duniani ilikuwa ikiratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Ukimwi (UNAIDS). Mwaka 2005 UNAIDS ililipa shirika lisilo la kiserikali la Kampeni ya Ukimwi Duniani (the World AIDS Campaign) wajibu wa kuratibu siku hiyo.
Kila mwaka siku hiyo hufanyika kwa ujumbe maalumu. Ujumbe wa mwaka 2005 hadi mwaka 2010 ulikuwa, "Zuia Ukimwi: Timiza Ahadi".
Uratibu wa Mwitikio wa Taifa dhidi ya janga la UKIMWI |
Mkakati wa Pili wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (2008 – 2012)
Mkakati wa Pili wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NMSF) unahusu kipindi
cha kuanzia mwaka 2008 hadi 2012. Unaendeleza mafanikio na uwezo wa
Mwitikio wa Taifa wa Mapambano dhidi ya UKIMWI katika kipindi cha miaka
mitano kilichopita (kuanzia mwaka 2003 hadi 2007) na kupendekeza hatua
za kuchukuliwa ikiwemo mikakati ya kukabili vikwazo na matatizo
vilivyopita. NMSF huu unaelekeza mikabala, afua na shughuli
vitakavyofanywa na watendaji wote nchini. Mkakati huu umetayarishwa
baada ya mapitio makubwa na mchakato wa ushauriano chini ya maelekezo ya
wataalamu wa Kitaifa na Kimataifa.Mpaka sasa UKIMWI ni tishio kubwa la maendeleo ya Taifa na umetangazwa kuwa ni janga la Taifa. Athari yake inasababisha kuenea kwa mateso miongoni mwa watu binafsi, familia na jamii nchini kote. Hata hivyo kuna dalili za matumaini. Kulingana na taarifa na takwimu za hivi karibu ushamiri wa VVU hauendelei na hata kufikia kupungua kidogo katika sehemu nyingi za Tanzania. Juhudi za kinga na upatikanaji wa matibabu yanayofaa vimepunguza athari ya UKIMWI miongoni mwa watu walioambukizwa. Hata hivyo, bado kuna Watanzania zaidi ya milioni moja walioambukizwa VVU na maambukizo mapya yanatokea nchini kila siku. Ukubwa wa janga hili na jumla ya athari zake katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita bado vinaleta changamoto kubwa nchini, changamoto ambazo zinaweza kukabiliwa kwa njia ya kuongeza juhudi shirikishi.
Mafanikio na changamoto
Miaka mitano iliyopita ya Mwitikio wa Taifa wa Mapambano Dhidi ya UKIMWI iliongozwa na Mkakati wa Kwanza wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (2003-2007). Katika miaka hii, kumepatikana mafanikio makubwa yaliyochangia kuimarisha juhudi za Kitaifa.
Miongoni mwa mafanikio makubwa katika maeneo manne yaliyodhamiriwa ni haya yafuatayo:
Mazingira yanayowezesha (masuala mtambuko):
Wizara, Idara na Wakala na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeanzisha kiasi fulani cha afua kwa ajili ya waajiriwa wao na sekta zao; VVU na UKIMWI vimefungamanishwa katika Mpango wa Muda mrefu wa Kupunguza Umaskini (MKUKUTA); TACAIDS imeweza kuwa mratibu mkuu wa mwitikio wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI; Waratibu wa UKIMWI wameteuliwa katika Wizara, na Idara, Wakala na Mamlaka za Serikali za Mitaa zote na Kamati za Kudhibiti UKIMWI ziliundwa; Kamati Shirikishi za Kudhibiti UKIMWI zilianzishwa katika Wilaya zote na katika baadhi ya Kata na Vijiji na mafunzo yalitolewa kwa wanakamati; Wakala za Uwezeshaji za Mkoa zilianzishwa katika Mikoa yote na zimetoa msaada mkubwa kwa Wilaya na Jamii;
Cheo cha Naibu Waziri wa Maafa na VVU na UKIMWI kilianzishwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu; Umoja wa Wabunge wa Mapambano dhidi ya UKIMWI Tanzania ulianzishwa; Vyama vya Kiraia vingi vimekuwa vikijishughulisha na VVU na hivyo kutoa uelewa wa kutosha nchini vikiwemo vikundi vingi zaidi vya WAVIU; Fedha kwa ajili ya shughuli za VVU na UKIMWI ziliongezwa zaidi kutoka Serikali na Wahisani na fedha nyingi zaidi zilifikia jamii; Kulikuwa na upanuzi zaidi wa mfumo wa kufuatilia maambukizo ya VVU; Utafiti wa mara kwa mara ulifanyika kuhusu VVU na mwenendo (ukiwemo VVU na UKIMWI katika Utafiti wa Hali ya Afya ya Watanzania)na Utafiti wa Kiashirio cha VVU Tanzania; Kulikuwa na uunganishaji wa utoaji taarifa kuhusu VVU na UKIMWI katika mfumo wa afya; na Kulikuwa na uendelezaji na uanzishwaji wa mfumo wa ufuatiliaji kwa ajili ya shughuli zisizokuwa za afya (TOMSHA).
Kinga:
Matibabu ya maambukizo kwa ngono yaliongezeka katika hospitali na vituo vya afya vyote na asilimia 60 ya zahanati; Kumekuwa na ongezeko kubwa la upatikanaji wa kondomu za wanaume nchini (kutoka milioni 50 hadi milioni 150); Vituo vya Unasihi na Upimaji wa Hiari vimeongezeka zaidi ya mara tatu; Uzuiaji wa Uambukizo wa VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto umeongezeka hadi kwenye asilimia 12 ya hospitali na vituo vya afya; Kutokana na utafiti mbalimbali, kulikuwa na uthibitisho kwamba vijana wameanza kubadili mienendo yao ya ngono (ongezeko la kuchelewesha shughuli za ngono, wapenzi wachache wa ngono n.k.) na programu za uendelezaji wa afya shuleni zilipanuliwa, na; Sekta binafsi na zisizo rasmi zimejihusisha zaidi na mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kutoa programu za kinga na matunzo kwa waajiriwa na jamii kwa ujumla.
Matunzo na Matibabu:
Mpango maalumu wa Tiba ya Kuongeza Kinga ya Mwili umetekelezwa na zaidi ya WAVIU 70,000 wamepewa matibabu hadi mwisho wa 2006, na Miradi ya matunzo nyumbani imepanuliwa hasa na vyama vya kiraia.
Upunguzaji Athari:
Misaada iliongezeka kwa mayatima, watoto wanaoishi katika mazingira magumu na vikundi vingine vinavyoishi katika mazingira magumu; na Kulikuwa na uhusishaji wa WAVIU katika Mwitikio wa Taifa hasa Uraghibishi na upunguzaji wa unyanyapaa na ubaguzi.
Hata hivyo, katika mwitikio wa jumla, bado kuna changamoto nyingi zinazohitaji kushughulikiwa kwa miaka ijayo. Miongoni mwa changamoto hizo ni: Upungufu wa utashi wa kisiasa katika ngazi ya kati na ya chini pamoja na uwajibikaji wa mwitikio wa VVU;
Programu chache na hafifu za VVU katika Wizara, Idara, Wakala na Mamlaka ya Serikali za Mitaa hasa katika ngazi za mikoa, wilaya na kufikia jamii; Chombo cha uratibu cha Kitaifa chenye majukumu mengi (TACAIDS); Kutotambuliwa na kutotumika kwa kanuni ya “Dhana Tatu” katika ngazi ya Serikali kuu na Wilaya. Uhusishaji mdogo wa vyama vya Kiraia na WAVIU hasa katika mipango na utekelezaji wa mwitikio wa VVU kwenye ngazi ya Wilaya na jamii; Ucheleweshaji wa mara kwa mara na matatizo katika kutoa fedha kwa wakati kwa Wilaya na Jamii; Uwezo mdogo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wa kuandaa na kutekeleza mipango kabambe ya VVU na UKIMWI; Unyanyapaa na ubaguzi bado ni vya kiwango cha juu katika jamii; Juhudi za kinga hazikushughulikia kiasi cha kutosha masuala ya afya ya ujinsia na uzazi na mara nyingi hazikutekelezwa; Bado kumekuwa na matatizo ya matumizi sahihi na ya mara kwa mara ya kondomu na upatikanaji mdogo katika jamii nyingi za vijijini; Uenezaji mdogo wa juhudi za kinga katika maeneo ya vijijini, na; Upatikanaji wa Tiba ya kuongeza Kinga ya Mwili ulikuwa katika vituo vya mijini tu.