ZAIDI
ya vituo 600 vya kutolea chanjo vitatumika Mkoani hapa kutolea chanjo ya
Surua-Rubella kwa watoto wenye umri wa miezi 9 hadi miaka 15, kampeni itakayoanza tarehe 18 hadi 24 octoba, 2014 kwenye vituo vyote vya kutolea
huduma za afya, shuleni na vile vitakavyoandaliwa na halmashauri.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Kapteni (Mstaafu) Chiku Ghallawa akifungua mkutano wa Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi uliolenga maandalizi ya Kampeni ya chanjo ya Surua-Rubella |
Akizungumza kwenye Mkutano wa
kamati ya huduma ya Afya ya msingi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Kapteni (mstaafu) Chiku Gallawa
aliwataka viongozi wa dini wejitolee
kuwahamasisha wananchi katika maeneo mbalimbali ili waweze kuitikia wito
wa kushiriki katika zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
“Kila mtu kwenye nafasi yake
aweke jitihada stahiki kufanikisha zoezi hili, tuwaelimishe jamii kuachana na
imani potofu juu ya uvumi kwamba chanjo hizi zinamadhara, serikali ni makini
haiwezi kuruhusu chanjo yenye madhara kwa wananchi wake,” alisema Gallawa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Asha Mahita akizungumza kwenye Mkutano huo, muda mfupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa Gallaawa |
Wajumbe wa Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi Mkoa wa Tanga, wakifuatilia kwa makini mkutano huo. |
Wajumbe wa Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi Mkoa wa Tanga, wakifuatilia kwa makini mkutano huo (wawili mbele) pamoja na baadhi ya waandishi wa Habari Mkoa wa Tanga. |
Serikali
chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaendesha zoezi hilo kwa
kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la kuhudumia
Watoto Duniani (UNICEF) kwa lengo la kudhibiti magonjwa yayoweza kuzuilika
ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa kuboresha afya za wananchi.
Nae Mganga mkuu wa Mkoa wa Tanga
Asha Mahita, alisema pamoja na chanjo hii, watoto wenye umri wa miezi 6 hadi
59 watapatiwa matone ya Vitamini A huku dawa za minyoo zikitolewa kwa
wale walio na umri kunzia mwaka 1 hadi miezi 59 na utoaji wa chanjo ya dawa za
Matende na Mabusha litawahusisha wananchi wote walio na umri wa kuanzia miaka 5
hadi 100.
Awali
mwakilishi wa Wizara ya Afya nchini Dkt Ibrahim Maduhu alisema chanjo hiyo ina
umuhimu mkubwa kwa wanawake wenye umri wa kuzaa na wajawazito kwa kuwa
itawakinga na athari ya kuzaliwa na ngozi yenye vipele, homa, tatizo la mtoto
wa jicho, mtindio wa ubongo, ulemavu na tatizo la Moyo.
Kampeni ya chanjo hii kitaifa itazinduliwa siku hiyo ya
Oktoba 18 ambapo zaidi ya asilimia 46 watanzania wanatarajiwa kunufaika ambapo
kaulimbiu ya mwaka huu ni “Linda, Okoa maisha ya Mtoto-kamilisha chanjo”.
No comments:
Post a Comment