MWANAMKE MAKINI BLOG

Advertise Here

Monday 13 October 2014

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA TANGA LEO 13/10/2014


Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Omary Salim mwenye umri wa miaka 42mkazi wa Tanga na mlinzi wa kituo cha mafuta cha Lake Oil cha Kange jijini Tanga ameuawa kwa kupigwa na nyundo kichwani na kuporwa silaha aina ya shortgun ikiwa na risasi mbili.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga Frasser Kashai

Katika tukio hilo pia amejeruhiwa mlinzi mwingine aitwaye Elisha Yohana mwenye umri wa miaka 48 mkazi wa Kange Kasera kwa kupigwa sehemu mbali mbali za mwili na kisha kufungwa kwa kamba.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Polisi mkoani hapa, Frasser Kashai amesema tukio hilo limetokea mnamo tarehe 10 octoba mwaka huu majira ya saa 8 usiku huko maeneo ya Kange Kata ya Maweni Tarafa ya Pongwe Wilaya ya Tanga mjini katika kituo cha mafuta cha Lake Oil.

Aidha Kamanda Kashai alisema majeruhi amelazwa hospitali ya Bombo na hali yake inaendelea vizuri na msako na upelelezi wa tukio hilo unaendelea

Muheza
Mwili wa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Saida Salimu mwenye umri wa miaka 62 mkulima na mkazi wa Bumbuli umegundulika ukiwa umeharibika  baada ya kuuawa kwa kukatwa na panga mgongoni na mtu/watu wasiofahamika wakati akiwa shambani.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Frasser Kashai amesema tukio hilo limetokea mnamo tarehe 10 octoba mwaka huu majira ya saa 1 jioni huko Mibuyu Mitatu Kitongoji cha Buhosi Kata ya Mtindiro tarafa ya Muheza Wilaya ya Muheza.

Hata hivyo Kamanda Kashai alisema kwamba mwili wa marehemu umezikwa na msako mkali wa kuwatafuta waliohusika na mauaji hayo unaendelea.

Handeni
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Peter Simba mwenye umri wa miaka 45 Mmasai mchunga Ngombe na mkaazi wa kijiji cha Nyasa ameuawa kwa kukanyagwa shingoni na kupigwa kwenye paji la uso na mchunga Ngombe mwenzake aitwaye Modest Martin mwenye umri wa miaka 32 mkazi wa Nyasa.

Akithibitisha  kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa Frasser Kashai alisema  tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 12 octoba mwaka huu majira ya 4 asubuhi huko katika kijiji cha Legazi Kata ya Nyasa Tarafa ya Magamba Wilaya ya Handeni.

Aidha kamanda Kashai alisema chanzo cha mauaji hayo ni kugombea sehemu ya kunywesha mifugo na maiti hiyo inafanyiwa uchunguzi na madaktari na itakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi mara baada ya uchunguzi wa madaktari kukamilika.

Sambamba na hayo kamanda Kashai alisema mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.

Jeshi la polisi mkoa wa Tanga linatoa rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa kuwafichua wahalifu wote kwenye maeneo yao wanayoishi ili wananchi wema ambao ndiyo walio wengi waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo bila usumbufu.

Taarifa
Jeshi la polisi mkoani hapa linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji ya binti aliyejulikana kwa jina la Blandina Bendera mwenye umri wa miaka 28 tukio lililotokea mnamo tarehe 13 September mwaka huu barabara ya 3 jijini Tanga.

Akizungumza na kituo hiki Kamanda wa polisi mkoani hapa Frasser Kashai alisema wanaoshikiliwa ni Andrew Augustino 28 mkulima na mkazi wa Mikanjuni na Jesse Kajuna 30 mkazi wa Mabawa na wote ni wakaazi jijini la Tanga.

Kamanda Kashai alisema watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya upelelezi wa awali kufanyika ambapo wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayo wakabili baada ya upelelezi kukamilika.

No comments:

Post a Comment