MWANAMKE MAKINI BLOG

Advertise Here

Wednesday 29 October 2014

TANZANIA KINARA NDOA, MIMBA ZA UTOTONI



TANZANIA ni moja ya nchi zinaoongoza kwa mimba na ndoa za utotoni, kwa mujibu wa ripoti inayotarajiwa kuzinduliwa jijini Dar es Salaam na Shirika la Haki za Binadamu duniani.

Hata hivyo nchi hiyo imepiga marufuku ndoa hizo, ambapo mtoto wa kike anaruhusiwa kuolewa anapofikisha umri wa miaka kumi na nane.
Mkoa wa Shinyanga ulio kaskazini magharibi mwa Tanzania ndio unaotajwa kuongoza kwa mimba na ndoa za utotoni, ikilinganishwa na mikoa mingine nchini.

Takwimu kutoka mashirika mbalimbali ikiwemo UNICEF zinaonyesha kuwa, kwa siku, watoto 16 wanapachikwa mimba za utotoni.

Kwa mujibu wa wataalamu, hali hii imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu na kwa asilimia kubwa imezorotesha maendeleo ya mtoto wa kike katika eneo hilo.

Ili kumwokoa mtoto wa kike kutokana na janga hili, kumekuwa na jitihada mbalimbali kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali za kuwaokoa hasa wale ambao tayari wameshatumbukia katika dimbwi hilo.

Shirika lisilo la kiserikali la Agape limeweza kuwaokoa wanafunzi wa kike wapatao mia mbili, wakiwa wamepitia ndoa za utotoni. Wengine tayari wamezalishwa wakiwa na umri chini ya miaka 13. Hivi sasa wanaanza maisha mapya ya kusoma.

Mmoja wa watoto waliokolewa akiwa amejitambulisha kwa jina la Pili Omar, ana miaka 14 na ni mama wa mtoto mmoja. na amekubali kueleza kilichomsibu.

"Niliolewa kwa sababu wazazi wangu waliniambia sitaendelea kuwa mzigo kwao, hivyo niolewe ili nianzishe mji wangu."anasema Pili.

Wazazi na walezi wa watoto hawa wanalaumiwa kwa kuwalazimisha watoto wao kuingia katika ndoa za utotoni. Licha ya kukithiri kwa ndoa hizo, pia imebainika kwamba asilimia 99 ya ndoa hizo hazidumu. 

Harieth Kulwa ni mmoja wa waathirika wa ndoa hizi ambaye ndoa yake imevunjika."Nilidhai kuolewa ndio kutatatua matatizo yangu, kumbe nilijiongezea matatizo. Mwanamume aliyenioa kwanza alikuwa mkubwa kwangu, pili alikuwa mlevi…" Anabainisha Harieth.

Hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu wanaulalamikia mfumo mzima wa kusimamia sheria kwa kutowachukulia hatua kali za kisheria watu wanaobainika kuwasababishia mimba watoto, wakidai kuwa ni kutokana na vitendo vya rushwa vilivyogubika vyombo vya sheria.

BURIANI RAIS MICHAEL SATA



RAIS wa Zambia, Michael Sata, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika hospitali ya London alikokuwa akitibiwa ugonjwa ambao haujatajwa.
Kifo chake kimetokea siku chache baada ya Zambia kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliingia madarakani mwezi Septemba 2011 baada ya kuongoza chama chake cha Patriotic Front, na kumshinda Rupiah Banda, ambaye alikuwa rais wakati huo na chama chake cha Movement for Multi-Party Democracy, kikiwa madarakani kwa miaka ishirini.

Michael Chilufya Sata alizaliwa mwaka 1937 katika mji wa Mpika, eneo ambalo lilikuwa wakati huo ni Northern Rhodesia. Muumini wa dini ya Kikristo ya madhehebu ya Katoliki, alifanya kazi kama afisa polisi, mfanyakazi wa reli na mwanachama wa chama cha wafanyakazi wakati wa utawala wa kikoloni. Baada ya Zambia kupata uhuru wake, pia aliishi kipindi fulani mjini London, akiwa mfanyakazi wa reli, na kurejea Zambia, akiwa na kampuni ya teksi.

Akiwa mwenye sauti ya mkwaruzo yakiwa ni matokeo ya kuvuta sigara kwa muda mrefu, Bwana Sata aliibuka katika siasa na kupata umaarufu katika miaka ya 1980.

Haraka akapata sifa ya kuwa gavana mwenye kuchapa kazi kwa bidii, wakati akiongoza jimbo la Lusaka na mtu wa utekelezaji kwa vitendo.
Lakini pia alijulikana kama mtu wa kutoa amri, mtu asiyeendekeza urafiki na mkali- na wapinzani wake walisema jina alilopewa la bandia la "King Cobra" alikuwa anastahili kuitwa hivyo.

Kwa mara ya kwanza alionekana kama mtu ambaye angetekeleza ahadi za kupambana na rushwa na kupata ufumbuzi wa tatizo la ajira na kuleta ustawi wa jamii. Lakini kipindi chake madarakani kiligubikwa na kuuzima upinzani wa kisiasa na kudorora kwa uchumi.

Bwana Sata ni rais wa pili wa Zambia kufariki dunia akiwa madarakani.

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA TANGA KWA VYOMBO VYA HABARI



KUJINYONGA
MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Biasin Isaa 35 mkulima na mkazi wa Mdolwa Bali Kutu amefariki dunia baada ya kujinyonga kwenye mti wa maembe karibu na nyumbani kwake kwa kutumia Khanga.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Naibu wa Kamanda wa polisi mkoani hapa Juma Ndaki amesema tukio hilo limetokea mnamo tarehe 27 octoba mwaka huu  majira ya saa 5 huko Mdolwa kijiji cha uuga Bazo Kata ya uuga na Tarafa ya soni Wilaya ya Lushoto .

Aidha Naibu wa kamanda Ndaki amesema chanzo cha kifo cha marehemu huyo ni msongo wa mawazo  na mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidiwa kwa ajili ya mazishi.

KUCHOMWA
MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Francis Mwendi Mkaburu 70 mkulima na mkazi wa kijiji cha Nyamaleni amefariki dunia baada ya kuchomwa moto akiwa ndani ya nyumba yake na watu wasiojulikana.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Naibu wa Kamanda wa polisi mkoani hapa Juma Ndaki amesema tukio hilo limetokea mnamo tarehe 28 octoba mwaka huu majira ya 1 huko kijiji cha Nyamwela kata ya Pagwi na Tarafa ya Kwekivu Wilaya ya Kilindi.

Sambamba na hayo naibu wa kamanda Ndaki amesema chanzo cha mauaji hayo ni kuhusiana na imani za kishirikina.

Pia Naibu wa kamanda Ndaki amesema msako mkali unaendelea katika kubaini watuhumiwa waliohusika na tukio hilo.

Sunday 26 October 2014

LUNDENGA ATOA YA MOYONI KUHUSU MREMBO WAKE SITTI MTEMVU KUJIVUA TAJI





MKURUGENZI wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga, amekanusha uvumi uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii mapema jana usiku, kuwa Sitti Abbas Mtemvu (pichani katikati) amelazimika kuvua taji la Urembo la Tanzania (Redd’s Miss Tanzania 2014).

Uvumi wa Sitti kuvua taji hilo umetokana na taarifa zilizotolewa kupitia akaunti ya Facebook mrembo huyo anayelalamikiwa kughushi vyeti vya kuzaliwa, akisema kutokana na vidole vya lawama anavyonyooshewa kiasi cha kukosa amani, amelazimika kuvua taji ili awe huru.

“Habari za jioni Watanzania wenzangu, kutokana na kuwa nimekuwa nikisemwa sana, maneno mengi yasio na tija juu ya hili taji la U-Miss anzania 2014,,mpaka kupelekea nisiwe na amani na uhuru ndani ya nchi yangu Tanzania, kwa roho safi nimeamua mwenyewe kujivua taji hilo na kuacha wanayeona anastahili taji hili apewe ili niendelee na maisha yangu kwa amani ,isiwe shida sana kwani sitegemei taji hili ili kuishi!!” imeandikwa katika ukurasa huo.

Akizungumzia uvumi huo, Lundenga alisema hakuna ukweli juu ya taarifa hiyo, na kwamba kama lingekuwa na ukweli ni wazi kwamba Sitti angeiarifu kampuni yake, inayoratibu kinyang’anyiro hicho kilichotimiza miaka 20 mwaka huu.