FAMILIA ya watu 18
wakiwemo watoto 10 na akina mama Nane mtaa wa Juma 50 kata ya Mwembesongo eneo
la Mafisa Msamvu Kilabu cha Makondeko Manspaa ya Morogoro wako hatarini
kukumbwa na magonjwa ya mlipuko na uambukizo baada ya kutupiwa vitu vyao nje ya
nyumba kwa madai ya amri ya mahakama.
Wakizungumza na mwandishi wa habari
hizi nyumbani hapo, baadhi ya wanafamila hao Magreth Kainyingi na
Adistela Kainyingi walisema tukio hilo walichofanyiwa Desemba 23 limelenga
kuwadhalilisha,kuwafedhehesha na kuwadhoofisha kimaendeleo kwakua hapo ni kwao
kihalali.
Walisema chimbuko la mgogoro huo ni
deni wasilolitambua la shilingi 800,000 walilokopeshana kati ya baba yao na mtu
waliemtaja Josia Masini aliebadili dhana ya mkopo nakuwa malipo ya ununuzi wa
nyumba hiyo.
Katika ufafanuzi huo Magreth alisema
mbali na vielelezo vya hati miliki walivyonavyo katika eneo hilo Ploti namba 35
kitalu ‘A’Msamvu,na kuthibitishwa na vyombo vya usimamizi ikiwemo Manspaa bado
Mahakama imekuwa ikipinga uhalali wake na kumpatia haki Masini.
Wakizungumzia kutupwa nje kwa mizigo
yao walisema Desemba 23 walivamiwa na watu wasiowajua waliojitambulisha kuwa
wafilisi wa mahakama kisha kuanza kubeba mizigo na kuitoa nje huku wakiwataka
kulipa shilingi 900,000 kama usumbufu.
Kwa nyakati tofauti imefikia Masini
akishirikiana na uongozi wa mtaa amekuwa akiwakamata kuwafikisha polisi na
mahakamani na tayari alishawahi kuwafunga jela mwaka mmoja na kazi ngumu wakiwa
na watoto wadogo.