BAADHI ya wananchi wa wilaya ya
Kilindi mkoani Tanga wataanza kunufaika na nishati ya umeme utokanao na kinyesi
cha ng’ombe hatua ambayo itawawezesha kumudu gharama za maisha njia ambayo pia
imeelezwa kuwa itasaidia kupunguza vitendo vya uharibifu wa mazingira kwa
kutojihusiaha na ukataji miti ovyo ili kupata kuni na mkaa.
Juma Kilo ambaye ni mwezeshaji
kupitia shirika la NCRF alimweleza mwandishi wa habari hizi juzi kuwa tayari
amefanikiwa kuwapatia elimu baadhi ya wananchi wa wilaya ya Kilindi na
wamehamasika kutumia nishati hiyo ambapo sasa utaratibu unaandaliwa ili kuweza
kufungiwa mitambo inayohusika.
Kilo ambaye ni mkazi wa kata ya
Mnyuzi wilayani Korogwe ambaye naye anatumia nishati hiyo katika familia yake
mara baada ya kupatiwa elimu kabla ya kuwa mhamsishaji kutokea wilayani Korogwe
alivitaja vijiji ambavyo watu wake wameelimishwa ni Songe, Kwinji, Kilindi,
Mafisa na Kilindi yenyewe.
Kuhusu gharama za mitambo ya umeme
wa kutumia kinyesi Kilo alisema kuwa kwa mtambo mdogo inatakia kiasi cha Tsh
700,000/= huku ul e mkubwa ukichukua Tsh 1.2 mil ambapo malighafi zinazotumika
katika ujenzi ni saruji, mawe na mchanga huku akisistiza kuwa uendeshaji wake
hauna gharama.
Mbali na kuzungumzia suala la
uenezaji wa nishati hiyo ya umeme wa kinyesi, Kilo alisema tayari wamegundua
mbolea bora ya yenye tija isiyo haribu ardhi inayotokana na kinyesi hicho
ambapo taratibu mbalimbali zinafanyika katika kuizalisha na hivyo kuleta mazao
yenye tija na ubora kwa wakulima.
Alisema kuwa mbolea hiyo haina
kemikali ambazo huharibu mazingira ila ni rafiki wa mazingira na hivyo jamii
kuwa na uhakika wa kuwa na mazingira yaliyo salama katika kipindi chote cha
maisha yao ambapo aliwashauri wananchi kuzitembelea ofisi za NCRF Korogwe ili
kupatiwa ushauri utakaowasaidia.
Mhamasishaji huyo aliendelea kusema
kwamba tayari soko la mbolea hiyo inayozalishwa kwa kinyesi cha ng’ombe ni
kubwa na bei yake ni yenye faida kubwa huku akiyataja naadhi ya maeneo ambayo
mradi wa NCRF umefika kuwa ni Pongwe nje kidogo ya jiji la Tanga, Muheza,
Usangi, Lushoto na Mkinga.
No comments:
Post a Comment