Msemaji wa TFF, Boniphace Wambura
TAIFA STARS KWENDA HARARE ALHAMISI
Msafara wa watu 30 wa Taifa Stars
unaojumuisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi unaondoka kesho alfajiri
(Mei 29 mwaka huu) kwenda Harare, Zimbabwe kwa ajili ya mechi ya marudiano ya
michuano ya Afrika.
Mechi hiyo itachezwa Juni Mosi mwaka
huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Harare, Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager itatua jijini humo saa 5 asubuhi kwa ndege ya Kenya
Airways.
Msafara wa Taifa Stars ambayo ambayo
jana (Mei 27 mwaka huu) ilicheza mechi ya kujipima nguvu na Malawi na kushinda
bao 1-0, na utarejea nchini Juni 2 mwaka huu unaongozwa na Rais wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.
Wakati huo huo, mechi ya kirafiki kati
ya Taifa Stars na Malawi (Flames) iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
imeingiza sh. 8,380,000 kutokana na watazamaji 1,504 waliokata tiketi
kushuhudia pambano hilo.
Mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 1,278,305.08, gharama za kuchapa tiketi sh.
225,600, gharama za uwanja sh. 1,031,414.24, gharama za mechi sh. 1,375,218.98
na TFF/Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 4,469,461.69.
MWAMBUSI KOCHA BORA VPL 2013/2014
Kocha Mkuu wa timu ya Mbeya City, Juma
Mwambusi ameshinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa msimu wa
2013/2014.
Hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi
mbalimbali ilifanyika jana (Mei 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, ambapo
mgeni rasmi alikuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mbali ya tuzo hiyo, Kocha Mwambusi
ambaye hivi sasa yuko nchini Sudan na timu yake kwenye michuano ya Nile Basin
alipata pia zawadi ya kitita cha sh. milioni 7.8.
Aliyeshinda tuzo ya kipa bora ni
Hussein Shariff wa Mtibwa Sugar aliyepata sh. milioni 5.2 wakati Amisi Tambwe
wa Simba aliibuka na tuzo ya mfungaji bora. Tambwe naye alipata sh. milioni
5.2.
Mchezaji bora wa VPL kwa msimu wa
2013/2014 ni Kipre Tchetche wa Azam FC aliyejipatia sh. milioni 5.2. Tuzo ya
refa bora imetwaliwa na Israel Mujuni aliyezawadiwa sh. milioni 7.8.
Yanga iliyoshika nafasi ya pili kwenye
ligi na kupata sh. milioni 37, pia ilipata sh. milioni 16 baada ya kushinda
tuzo ya timu yenye nidhamu ya hali ya juu. Sh. milioni 21 za mshindi wa nne
zilikwenda kwa timu ya Simba.
Mabingwa wapya wa VPL, Azam FC walipata
sh. milioni 75 wakati Mbeya City ilipata sh. milioni 26 kwa kushika nafasi ya
tatu.
RAIS MALINZI ATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA
KOCHA
Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za
rambirambi Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya
kutokana kifo cha Kocha wa timu ya Nkana FC, Masauso Mwale.
Amesema
amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha ghafla cha Kocha Mwale, na kuongeza
kuwa msiba huo si pigo kwa Zambia pekee bali Afrika kwa ujumla kwa vile ni mfano
wa kuigwa kwa makocha wazalendo waliozipatia mafanikio makubwa klabu za Afrika.
Rais Malinzi
amemuomba Rais Bwalya kutuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Mwale, na
kuitaka kuwa na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito
kwao.
Mwale (51)
alifariki mwishoni mwa wiki kwa ajali ya gari aliyokuwa akiendesha katika
barabara ya Kitwe- Ndola akienda kambini kujiunga na timu yake kwa ajili ya
maandalizi ya mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Sewe San Pedro ya Ivory
Coast.
No comments:
Post a Comment