MWANAMKE MAKINI BLOG

Advertise Here

Thursday, 18 December 2014

MAMA KIKWETE: VIJANA MJIUNGE VIKUNDI VYA KUWEKA NA KUKOPA

VIJANA wametakiwa kujiunga na vikundi vya kuweka akiba na kukopa  ili kuchangia mawazo yao  na ubunifu na wakati huo huo wanajitengenezea mazingira ya kujiajiri kwani wengi wao wana elimu na ujuzi walioupata  masomoni lakini wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira.
 
Rai hiyo imetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akizindua Umoja wa Vikundi vya kuweka Akiba vilivyopo chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wilaya ya Kinondoni (UWAMAKI) katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Usafirishaji jijini Dar es Salaam. 

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA alisema kupitia vikundi hivyo vijana wanaweza kupata mitaji midogomidogo pamoja na mafunzo ya kuwawezesha kuanzisha biashara na kujiajiri. Kwani mfumo huo wa vikundi na mafunzo ni moja ya njia za kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na hivyo kupunguza tatizo la ajira.

Kwa upande wa wanachama wa UWAMAKI aliwasisitiza  kutoridhika na mafanikio waliyoyapata bali waendelee kutafuta njia za kupiga hatua hususani kupata utaalamu wa kuboresha bidhaa zao , kutafuta masoko zaidi na kufanya ubunifu wa kuweza kuvumbua bidhaa na biashara nyingine tofauti ili kuepukana na ushindani wa soko.

“Mnapokuwa na bidhaa zinazofanana mtakuwa katika mazingira ya kushindania soko jambo ambalo litapunguza kiasi cha mauzo ambayo ndiyo pato lenu wajasiriamali. Jitihada ifanywe ili kuweza kutafuta watalaam ambao watawapa mafunzo ya kukuza biashara”, alisema Mama Kikwete. 

Akisoma risala ya vikundi hivyo Katibu wa UWAMAKI , Mwajuma Waziri aliishukuru Taasisi ya WAMA kwa kuwawezesha  kuwa na vikundi na kupata mafunzo ya kuweka akiba, elimu ya kibenki, usindikaji wa vyakula na huduma ya bima ya afya. 

Waziri alisema, “Kutokana na mafunzo hayo tunaweza kuanzisha miradi mbalimbali kama vile kutengeneza sabuni za maji za kufulia, sabuni za kuoshea vyombo na kusafishia tairizi, siagi ya karanga na batiki na hatimaye tumeweza kufungua akaunti yetu ya Umoja katika benki ya wanawake (TWB)”.

Katibu huyo alisema walianza na kikundi kimoja kwa kujiwekea hisa moja kwa thamani ya shilingi 1000 pia waliweza kukopesha kiasi cha shilingi 6,300,000 mpaka mwisho wa mwaka walivuna shilingi 12,750,000. 

“Hadi sasa tunavikundi 11 vyenye wanachama 274 kati ya hao wanaume ni wanane katika vikundi hivi  tumeweza kukopesha kiasi cha shilingi 47,500,000/= na kufikia mavuno ya shilingi 79,739,000 kwa mwaka”, alisema.
Alimalizia kwa kusema lengo la kuunda umoja huo ni kushirikiana katika matatizo ya kijamii, kuunda SACCOS na kutafuta masoko ya bidhaa zao.

Taasisi ya WAMA inasimamia mradi wa kuwawezesha wanawake kwa kuwapa mafunzo kupitia vikundi katika mikoa ya Dar es Salaam Lindi na  Pwani hadi kufikia Septemba mwaka huu jumla ya watu 18,000 wamefikiwa kwa kupitia vikundi 688 vilivyoundwa na tayari shilingi milioni 227 zimekusanywa na kukopeshwa.

RAIS ATEUA MKURUGENZI MTENDAJI SHIRIKA LA MAENDELEO YA PETROLI (TPDC)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Dkt. James P. MATARAGIO kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kulingana na, Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue uteuzi huo ulianza tarehe 15 Desemba, 2014.

Dkt. James P. MATARAGIO ni Mtanzania ambaye hivi sasa anaishi na kufanya kazi nchini Marekani akiwa Senior Geoscientist wa Kampuni ya Bell Geospace, Houston, Marekani. Wasifu wake ni kama ifuatavyo:-

ELIMU:- • Masters in Business Development (MBA), Chuo Kikuu cha Charlotte, North Caroline, Marekani (2008) • PhD (Geochemistry, Mineralogy, Structural Geology and Petroleum Geology), Chuo Kikuu cha Missouri – Rolla, Missouri, Marekani (2005) • MSc (Geochemistry and Petrology), Chuo Kikuu cha Okinawa, Japan (1997) • BSc(Hons) (Geology), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1994

UZOEFU WA KAZI:-
• Mwaka 2004 – hadi sasa, Senior Geoscientist, Bell Geospace Inc, Houston, Texas, USA • 2001 – 2004, Mhadhiri Msaidizi, Chuo Kikuu cha Missouri, wakati akisoma Shahada ya Uzamivu • 2000 – 2001, Mhadhiri Msaidizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. • 1999 – 2000, Meneja Mradi, Anglo Gold (Buzwagi) • 1994 – 1999 -, Exploration Geologist, Anglo America Corporation.

Miongoni mwa makampuni makubwa ya kimataifa ya mafuta na gesi aliyofanya nayo kazi kwa niaba ya mwajiri wake Bell Geospace ni pamoja na Petrobras (Brazil); BP; Anadarko; Tullow; Pemex (Mexico); ANP (Brazil), Ecopetrol (Colombia); Petronas, (Malaysia) na Vale Rio Doce.

Aidha, Dkt. James P. MATARAGIO ni mmoja wa wataalam wa sekta ya madini, mafuta na gesi asilia waishio Marekani (Diaspora) ambao walijitolea kuishauri Serikali kuhusu sekta hiyo bila malipo.

​Kwa kuzingatia elimu yake, uzoefu wake na uzalendo wake, Rais ana matumiani makubwa kuwa Dkt. James P. MATARAGIO ataleta nguvu mpya na uzoefu mkubwa wa kimataifa katika kuiongoza TPDC ili iwe kampuni kubwa ya kitaifa ya mafuta na gesi asilia kama yalivyo makampuni mengine ya kitaifa ya mafuta na gesi asilia duniani.

Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
18 Desemba, 2014

Tuesday, 16 December 2014

KITUO CHA AFYA PONGWE KIMEPOKEA TUZO YA BIMOC


WIZARA ya afya na Ustawi wa Jamii imetoa tunzo ya BIMOC kwa Kituo cha afya cha Pongwe pamoja na vyeti maalum vya daraja la kwanza. 


Hatua hii imekuja baada ya kuridhika na  huduma bora  ya dharura kwa wanawake wajawazito na watoto inayotolewa na kituo hicho.


Akifafanua maana ya BIMOC katika hafla fupi iliyofanyika kituoni hapo hii leo mganga mkuu Faisal Ally, mara baada ya kupokea tunzo hiyo amesema hiyo ni kuonyesha kuwa kituo hicho ni bora kwa huduma ya mama na mtoto


Sanjari na hayo pia Mganga huyo ameelezea uwezo mwingine walionao kituoni hapo kama vile kufanya upasuaji, kutoa dawa za usingizi, huduma ya kutoa na kuhifadhi damu salama ambayo wanategemea kuianza hivi karibuni baada ya kukamilika kwa mahitaji ya vifaa kadhaa.

Hata hivyo changamoto inayowakumba katika kutoa huduma kwa mama wajawazito ambayo hutolowa bure ameelezea kuwa ni urejeshaji wa matumizi wanayotumia kuwahudumia 

ASKARI WALIOSIMAMIA UCHAGUZI MDOGO TANGA BADO HAWAJALIPWA



ASKARI Mgambo wapatao 200 wameilalamikia ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Tanga kwa kutowalipa fedha zao kama malipo kwa kazi ya usimamiaji zoezi la kupiga kura.

Baadhi ya askari hao MG 427805, MG 351976 na MG 265079 wakizungumza na Redio Huruma kwa niaba ya wenzao walipofika ofisi za Jiji la Tanga wamesema licha ya kuelekezwa kumfuata Mkurugenzi Juliana Malange ili awezeshe malipo hayo zaidi ya mara mbili juhudi zao zimegonga mwamba bila kupatiwa majibu ya kina.

Mwandishi wetu Rebecca Duwe alizungumza na Mkurugenzi kwa njia ya simu ambeye naye aliyolea ufananuzi huu suala hilo kuwa yeye siye aliwewapangia vituo hivyo itamuwia vigumu kuwatambua.

Ameongeza kwamba ni vyema wakawasiliana na OCD ambaye atawasilisha majina kwane ili aweze kukamilisha hayo malipo kwasababu fedha zipo kwa ajili ya kufanya hivyo.

Hata hivyo wenzao (waalimu) tayari walipatiwa malipo yao hata kabla ya zoezi kuanza.

DOSARI ZA UCHAGUZI MDOGO KUREKEBISWA DEC 21



UCHAGUZI wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika jana nchini ulitawaliwa na dosari ambapo Mkoani Tanga katika baadhi ya maeneo yamelazimika kuahirisha zoezi la upigaji kura hadi DEC 21, 2014.

Maneneo ambao uchaguzi haukuenda sawa na aina ya viongozi ambao hawakuchagulia ni Kata ya Ngamiani Kati mitaa mitano kwa nafasi ya viti maamulu, Duda mitaa minne uchaguzi wa viti vitimaalumu maeneo yote haukufanyika, Majengo C wajumbe mchanganyiko hawakuchagulia, Pongwe kati wajumbe mchanganyiko, na Kata ya Kiomoni hawakuchagua Mwenyekiti, wajumbe na viti maalumu.

Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Juliana Malange amezungumza na Mwanamkemakini  juu ya sababu zilizosababisha kutofanyika uchaguzi huo kuwa ni kasoro zilizojitokeza kwenye karatasi za kupigia kura.

Aidha taarifa ya matokeo kwa maeneo walio piga kura ambapo CCM kwa nafasi ya mwenyekiti mitaa 118, CUF mitaa 60, Chadema mitaa 2, kwa nafasi ya Wajumbe mchanganyiko CCM 356, CUF 117 na Chadema 3, Vitimaalumu CCM 230, CUF 162 na Chadema 2.

“Katika uchaguzi huu kwa nafasi ya mwenyekiti CCM ilishinda kwa 65%, CUF 33% na Chadema 1%.

Friday, 12 December 2014

ESCROW KUIKOSESHA TANZANIA TRILIONI 1.1 ZA MCC



SERIKALI nchini hapa iko hatarini kukosa dola za Marekani milioni mia saba sawa na trilioni 1.1 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya mradi wa pili wa mfuko wa changamoto za Milenia (MCC) kutokana na kushamiri kwa vitendo vya rushwa nchini humo.

Marekani imebainisha kuwa mkataba wa pili wa miradi inayofadhiliwa na shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC) utategemea hatua zitakazochukuliwa na serikali ya Tanzania dhidi ya wahusika wa kashfa hiyo.

Haya yanajiri wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa kutoa maamuzi ya mapendekezo yaliyofikiwa na Bunge kuhusiana na sakata la uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka kaunti ya Tegeta Escrow wiki ijayo.

Katika tamko hilo kwa umma ambalo limewekwa kwenye tovuti ya MCC, bodi ilieleza kutambua umuhimu wa kusubiri na kuona utekelezaji kamilifu wa tamko lililotolewa na Ikulu ya Tanzania Desemba 9, mwaka huu kwamba itachukua hatua za haraka na kutoa maamuzi dhahiri na thabiti kuhusu maazimio ya Bunge juu la suala la IPTL.

Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ilieleza kuwa wakurugenzi wa MCC waliokutana katika mkutano wao uliofanyika Desemba 10, mwaka huu wamesikitishwa na hali ya rushwa nchini Tanzania.

Itakumbukwa Wakati wa mkutano wa 16 na 17 wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alidokeza kusudio la Marekani kukataa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya MCC, lakini Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikanusha taarifa hizo.

MCHUNGAJI AKEMEA WANAOITA WATOTO MCHUMBA, ASEMA NI UDHALILISHAJI



KIONGOZI wa Kanisa la KKKT Pemba Mchungaji Benjamini Kisanga amekemea tabia ya baadhi ya wazazi kuruhusu watoto wa Kike kuitwa mchumba hali ambayo inachagia kuwepo na matendo ya udhalilishaji wa Kijinsia.

Amesema kuwa kuruhusu mtoto wa kike kuitwa mchumba kunawajengea mazingira ya kuwazoea watu na hivyo kuwa ni rahisi kwa mtoto huyo kudhalilishwa.

Akizungumza na redio Huruma Kisiwa Pemba  kwenye maadhimisho ya haki za Binadamu , ameitaka jamii kuwalinda watoto wa kike kwa kuhakikisha kwamba wanakemea vitendo vya kuitwa mchumba.

Aidha Mchungaji huyo wa kanisa la KKKT amesema baadhi ya watu wanatabia mbaya na hivyo wanapata mwanya wa kutekeleza matendo hayo baada ya wazazi kukubali  watoto wao kuwa na mazoea na watu.

Hata hivyo ameishauri jamii kufuatilia mienendo ya watoto wao ili kuwalinda na makundi maovu ambayo ynaweza kuwa ni kishawishi cha kuharibu mustakabali wa maisha yao.